Friday, July 6, 2012

KAMATI YA BUNGE YAFANYA ZIARA MWANZA KUTANZUA MGOGORO WA SAMAKI: TUME YABAINI UOZO MWINGI..

Waziri wa mifugo na uvuvi mh. Mathayo David akizungumza na wadau wa samaki Mwanza kulia ni makamu mwenyekiti kamati ya kilimo, mifugo na maji ambaye ni Mbunge wa Vijana DSM Neema Mgaya na wa kwanza kushoto ni wajumbe wa kamati ya kilimo na mifugo Rose Kamili (Mbunge wa viti maalum CHADEMA - Manyara) na mh. Dr. Titus Kamani (Mbunge wa Busega).
Serikali imepiga marufuku uvuvi na uingizwaji wa samaki walio chini ya kiwango kuchakatwa ndani ya viwanda ikiwa ni pamoja na wamikili wake kujihusisha na uvuvi na ununuaji samaki kwenye mialo kanda ya ziwa Victoria.

Tamko hilo limetolewa jana na Waziri wa mifugo na uvuvi Mathayo David Mathayo wakati alipokutana na wavuvi, wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki katika kikao cha kujadili mgogoro uliosababisha wavuvi kugoma na viwanda kutetereka kiuzalishaji.

Wakurugenzi ambao ni wamiliki wa viwanda vya kuchkata samaki jijini Mwanza, kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Tanzania Fish Processor (TFP) Ganeshan Vedagir, Amini wa Omega Fish na Peter John wa Nile Perch Fisheries

Kuhusu mgogoro uliodumu takribani mwezi mmoja sasa Waziri David Mathayo, akiwa ameambatana na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Maji na Mifugo, amewashauri wavuvi kuanzisha ushirika wa pamoja utakao wasaidia kutambua bei halali, kudhibiti bei duni na mapungufu yasiyo ya lazima yanayojitokeza.

Mjumbe wa kamati ya kilimo na mifugo Rose Kamili (Mbunge wa viti maalum CHADEMA - Manyara) akiwasilisha jambo kwaajili ya kupata muafaka wa mgogoro baina ya wavuvi na wamiliki wa viwanda Ziwa Victoria, uliosababishwa na wamiliki wa viwanda kushusha bei ya samaki, kulia ni mh. Dr. Titus Kamani (Mbunge wa Busega).
Katika maazimio Kamati hiyo ya bunge imeshauri kuwepo kwa mikataba ya aina moja baina ya wavuvi na wamiliki ambayo itapitiwa na wanasheria wa pande zote mbili chini ya usimamizi wa serikali wakati wa kuandaliwa hatimaye utekelezwaji ili kuepuka migogoro ambayo ni chanzo cha migogoro kupitia dhuruma inayopelekea kuporomoka kwa pato la Taifa.

Mjumbe wa kamati mh. Moshi Selemani Kakoso (Mbunge wa mpanda vijijini) akitoa maelezo ili kupata ufafanuzi.
Suala kubwa lilikuwa ni bei wavuvi wakihitaji bei ipande angalau shilingi 5,000/= kwa kilo moja ya sangara lakini wenye viwanda wamesema kutokana na kushuka kwa ya bei kwenye soko la ulaya hawataweza kupandisha zaidi ya shilingi 3,200/= kwa kilo.


Licha ya kamati hiyo kuwasihi wamiliki wa viwanda kupandisha bei ili kukidhi gharama za mvuvi lakini kutokana na sababu walizoambatanisha wakakomea hapo.

Wavuvi kikaoni.
Tatizo la bei hatimaye mgomo halijawahi kutokea kwenye sekta ya samaki Kanda ya Ziwa lakini kutokana na mapinduzi ya viwanda na kutokuwa na chama cha Ushirika ambacho kingeweza kuwasemea na kunegotiate bei na wanunuzi wa samaki wavuvi imefikia wakati wamekuwa wakinyanyaswa kutokana na kutojua sheria.

Mjumbe wa kamati hiyo toka bungeni mh. Dr. Titus Kamani (Mbunge wa Busega).
Hivyo basi kamati hiyo imetoa mapandekezo kwa wavuvi kuandaa mchakato wa kuanzisha chama cha ushirika ambacho kitakuwa kikiwauzia samaki wenye viwanda na kusimamia bei.

Wakurugenzi wa viwanda mbalimbali Mwanza.
Umuhimu wa kuanzishwa kwa vyama vya Ushirika ulionekana katika Mikoa ya kusini nchini Tanzania ambapo wakulima walikuwa wakitaabika na soko la korosho, manufaa yalionekana mara baada ya serikali kuingilia kati na vyama vya ushirika kufufuliwa, vilivyokuwa havina uwezo wa kukopa vikawezeshwa hatimaye vikaweza kukopesha na hivi sasa vinanunua korosho na kuwauzia wanunuzi wengine kwa minada suala ambalo likivaliwa njuga na wavuvi wa samaki hakika litawapa manufaa.

Meza kuu mkutanoni kutoka kushoto ni wajumbe wa kamati ya kilimo na mifugo Rose Kamili (Mbunge wa viti maalum CHADEMA - Manyara) na mh. Dr. Titus Kamani (Mbunge wa Busega) wakiwa na Waziri wa mifugo na uvuvi mh. Mathayo David.

Suala lingine walilolalamikia wavuvi ni kwamba samaki anapo fikishwa kiwandani na kutajwa kuwa ni reject harudishwi na kiwanda hivyo kamati hiyo imetamka kuwa kama samaki ni reject basi arudishwe kwa mvuvi badala ya viwanda kuchukuwa reject hao.

Mkurugenzi wa Monarch Hotel Mwanza Osward m. Mwizarubi akizungumza na Waziri wa mifugo na uvuvi mh. Mathayo David mara baada ya kumalizika kwa majumuisho ya kutanzua mgogoro baina ya wavuvi na wamiliki wa viwanda vya samaki yaliyofanyika hotelini hapo.
Wavuvi hao wamelalamika kitendo cha wamiliki wa viwanda kutowaruhusu kuingia viwandani kushuhudia uzito na kupitia hilo kamati imesema wazi kuwa huo ni wizi hivyo imeagiza wanunuzi na wenye viwanda kuwaruhusu wavuvi kuingia viwandani kushuhudia upimwaji na kujua uzito halali wa mali waliyouza ili kupata haki zao.