Thursday, December 29, 2011

MBUNGE WA BUSEGA Dk. TITUS KAMANI, AMEJIPANGA KUWATUMIKIA WANANCHI

Tuesday, May 3, 2011Makamu wa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na aliyekuwa mgombea mwenza wa urais wa CCM katika uchaguzi uliopita Dk. Mohamed Gharib Bilal, akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Lamadi eneo la Nyamikoma Wilaya ya Busega, wakati alipofika katika Jimbo la Busega kufanya mkutano wa kampeni na kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk. Titus Kamani.

MBUNGE wa Busega Dk. Titus Kamani, amesema amejipanga kuhakikisha anawatumikia wananchi wake ili wapate maendeleo ya haraka.


Pia, amewashitakiwa kwa wananchi wake wanasiasa wanaompaka matope ikiwa ni mpango wa kuhakikisha anapoteza dira katika kutekeleza mipango ya maendeleo.


Hivi karibuni kumezuka kikundi cha wanasiasa waliokuwa wapinzani wa Dk. Kamani wakati wa mchakato wa kura za maoni, wakimpaka matope na kushawishi wananchi wasishiriki shughuli za maendeleo.


Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Nyashimo mjini Ramadi, juzi, ambapo alisema fitina zinazopikwa dhidi yake ni uendelezaji wa siasa chafu unaofanywa na wanasiasa wasiokubali matokeo.


Awali, kabla ya kuzungumza kwenye mkutano wa hadhara, mamia ya wananchi walijitokeza kumlaki Dk. Kamani wakati alipowasili mjini Ramadi pamoja na kumpongeza kwa kuchaguliwa Mwakilishi katika Bunge la SADC.


Alisema kuwa mikakati inayofanywa na wanasiasa kuhakikisha wanampaka matope kwa lengo la kumharibia sifa yake, si jambo zuri na halina budi kukemewa na wananchi wote wa Busega.


Hata hivyo, alisema kuwa hana muda wa kubishana na wanasiasa hao kwa kuwa uchaguzi ulishamalizika na kwamba, amejielekeza zaidi katika kuwatumikia wananchi wake na si kuendesha siasa za majitaka.


Aliwaasa wananchi kutokubali kurubuniwa na wanasiasa, ambao wana lengo la kuhakikisha wanakwamisha maendeleo jimboni humo ili kutaka kuonyesha kuwa hajawafanyia mambo mema wananchi wake.


Dk. Kamani alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa CCM kumlinda dhidi ya siasa chafu zinazoendeshwa dhidi yake na wanasiasa hao kwani, kwa sasa wamefikia hatua mbaya na isiyostahili kuvumiliwa. “Naomba CCM na viongozi wangu wanilinde juu ya mambo haya ninayofanyiwa… Nimeshinda kwa kura nyingi tena kwa kufuata taratibu zote na wananchi wamenikubali.


Kuanza kupakana matope kwa mambo mazito wakati uchaguzi ulishakwisha hakuna maana. Tushirikiane kukijenga Chama na kuwatumikia wananchi wetu. “Nimewaeleza haya wananchi wenzangu kwa kuwa ndiyo mlionipa hii nafasi ya kuwa mwakilishi wenu na mtaamua hatua za kuwachukuliwa hawa watu. Naomba muwaadhibu kwa kuwaeleza kuwa juu ya siasa chafu wanazonifanyia kuwa mmewabaini,” alisema Dk. Kamani.


Kuhusu kuchaguliwa mwakilishi wa Bunge la Tanzania katika SADC, Dk. Kamani alisema kumetokana na baraka alizopewa na wananchi wa Busega hivyo, atawatumikia mahali popote na muda wowote.

MKONGO WA TAIFA NA JIMBO LA BUSEGA

11 April 2011
Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri yanayotia moyo ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa hivi kuna Mkongo wa Taifa ambao umepitishwa ndani kabisa ya Jimbo la Busega ukipitia vijiji vya Kiloleni, Nasa, Kalemela na Lamadi na kuna kituo kimejengwa pale Nasa kwa ajili ya kutoa huduma .
Je, ni lini wananchi wa jimbo la Busega wataanza kunufaika na Mkongo huu wa Taifa? Ahsante.


NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Titus Kamani, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kabisa Mheshimiwa Dkt. Kamani kwa kutambua kwamba Mkongo wa Taifa umefika na umepita katika Jimbo lake kwa sababu pale Nasa lile jengo ni la zamani lakini kituo cha mawasiliano ya Mkongo wa Taifa kimewekwa kule ndani lakini ameweza kuitambua, kwa hivyo ni suala ambalo ningependa nimpongeze sana.


Mheshimiwa Spika, nimfahamishe tu Mheshimiwa Dkt. Kamani kwamba kituo kile kwa sasa kinatumika kama kituo cha kuwezesha mawasiliano au huduma ya Mkongo kuongeza yale mawimbi ya mawasiliano kupata nguvu zaidi.


Lakini katika awamu yetu ya tatu sehemu hiyo ya Nasa kituo hicho kitaweza kuwa na vitambuzi (intelligent gargets) ambavyo vitaweza kufikisha mawasiliano katika sehemu zingine kama pale Magu na Bunda.


Mheshimiwa Spika, lakini vile vile nipende tu kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika hali ya sasa hivi wananchi wa Busega wanazidi kupata nafuu ya mawasiliano kupitia makampuni mbalimbali ya simu kwa mfano Kampuni ya Airtel sasa hivi katika kutambua na kutumia Mkongo wa Taifa imeweza kushusha gharama za mawasiliano katika internet kutoka ilivyokuwa kwa 50% kwa hiyo sasa hivi wananchi wa Busega wanapata internet kwa punguzo la 50% na katika awamu ya tatu itafikisha huduma hizo katika wilaya na wananchi wengi wataweza kupata faida zaidi.