Thursday, December 29, 2011

MKONGO WA TAIFA NA JIMBO LA BUSEGA

11 April 2011
Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri yanayotia moyo ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa hivi kuna Mkongo wa Taifa ambao umepitishwa ndani kabisa ya Jimbo la Busega ukipitia vijiji vya Kiloleni, Nasa, Kalemela na Lamadi na kuna kituo kimejengwa pale Nasa kwa ajili ya kutoa huduma .
Je, ni lini wananchi wa jimbo la Busega wataanza kunufaika na Mkongo huu wa Taifa? Ahsante.


NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Titus Kamani, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kabisa Mheshimiwa Dkt. Kamani kwa kutambua kwamba Mkongo wa Taifa umefika na umepita katika Jimbo lake kwa sababu pale Nasa lile jengo ni la zamani lakini kituo cha mawasiliano ya Mkongo wa Taifa kimewekwa kule ndani lakini ameweza kuitambua, kwa hivyo ni suala ambalo ningependa nimpongeze sana.


Mheshimiwa Spika, nimfahamishe tu Mheshimiwa Dkt. Kamani kwamba kituo kile kwa sasa kinatumika kama kituo cha kuwezesha mawasiliano au huduma ya Mkongo kuongeza yale mawimbi ya mawasiliano kupata nguvu zaidi.


Lakini katika awamu yetu ya tatu sehemu hiyo ya Nasa kituo hicho kitaweza kuwa na vitambuzi (intelligent gargets) ambavyo vitaweza kufikisha mawasiliano katika sehemu zingine kama pale Magu na Bunda.


Mheshimiwa Spika, lakini vile vile nipende tu kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika hali ya sasa hivi wananchi wa Busega wanazidi kupata nafuu ya mawasiliano kupitia makampuni mbalimbali ya simu kwa mfano Kampuni ya Airtel sasa hivi katika kutambua na kutumia Mkongo wa Taifa imeweza kushusha gharama za mawasiliano katika internet kutoka ilivyokuwa kwa 50% kwa hiyo sasa hivi wananchi wa Busega wanapata internet kwa punguzo la 50% na katika awamu ya tatu itafikisha huduma hizo katika wilaya na wananchi wengi wataweza kupata faida zaidi.

No comments:

Post a Comment