DK KAMANI: AFUNGUKA,
AWATAKA WAFANYAKAZI WASIOENDANA NA KASI YAKE WAJIONDOE MAPEMA!
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dr. Titus Kamani,
amesema ili kwenda na kasi ya maboresho ya wizara hiyo, inahitajika dhana ya
uwajibikaji na uwazi sambamba na kujitolea kwa nguvu zote katika kufanya kazi.
Waziri Kamani, ameyasema hayo leo katika mkutano wa kwanza
uliowakutanisha wafanyakazi wote wa wizara hiyo, wakiwemo wastaafu wa mwaka
jana katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Temeke jijini Dar es Salaam .
Amesema kama kuna mtu ambaye ni kikwazo katika kukwamisha
shughuli za wizara, ni bora akawapisha mapema na kwamba kila mtumishi kwa
nafasi yake, anatakiwa kuifanya kazi kwa uwazi na akaitaka wizara kufanya kazi
na vyombo vya habari kwani ndio njia pekee ya kuwafanya watanzania wajue wizara
inafanya nini.
“Wewe upo ofisini, halafu unaogopa ogopa vyombo vya habari,
kwani unatatizo gani, kuweni wazi mambo yenu yawe hadharani, watanzania wa
Mbeya wayajue, Rufiji mpaka Pemba , hakuna
kufichaficha jambo katika wizara yangu.” Alisistiza Dk Kamani.
Amesema wizara ya maendeleo ya mifugo na uvuvi ndio moyo wa
taifa kwani huwajumuisha watanzania wengi wenye maisha ya kawaida, lakini
amesikitishwa kwa jinsi ambavyo wizara hiyo imekuwa ikichukuliwa na baadhi ya
watu kama ni wizara ya yenye migogoro na kuleta
hasara maeneo mengine.
“N’gombe hawa wamekua wakiingia kwenye hifadhi, wanapigwa
risasi, wanaaribu mashamba ya watu na kuleta njaa kwa wananchi, ngombe hawa
wamekuwa wakiambiwa wanaleta uharibifu wa mazingira kwa wananchi kwa sababu ya
kuhamahama, kama ngombe hawa ungepatikana utaratibu mzuri wa kuwatunza,
kuwahifadhi basi, taifa hili lingeingiza kipato kikubwa ikiwemo kuuza nyama
hadi nje ya nchi, maziwa na kuboresha afya za watanzania” alisema Dk Kamani.
Dk. Kamani, amesema anafahamu Wizara yake ina changamoto
nyingi katika kutekeleza majukumu yake, ikiwemo bajeti kuwa ndogo, lakini kwa
kutumia taaluma yake pamoja na ushirikiano wa wafanyakazi wote wa wizara hiyo,
anaamini wizara hiyo badala ya kuonekana ni laana kwa watanzania, itakuwa ni
wizara yenye neema kwa watanzania, yenye kueneza ajira na kipato kwa sababu
hakuna jambo lisilowezekana kama kila mmoja atafanya kazi kwa dhamira moja.
Akizungumzia juu ya ranchi za
taifa, waziri Kamani amesema ana nia ya dhati ya kuona ranchi za taifa zinafufuka na kutengeneza
uchumi imara wa taifa, kuzalisha Ngombe wenye ubora ambao watatoa mazao ya
mifugo yatakayoliingizia taifa hili kipato kikubwa.
Akizungumzia sekta ya uvuvi, Waziri Kamani, amesema sekta
hiyo ni tabu tupu, amesema leo tunaambiwa kuna uvuvi haramu, nyavu zisizokidhi
viwango, huku wavuvi wakiendelea kuwa masikini, katika nchi yenye bahari,
maziwa na mito
mikubwa kila kona, ameuliza ni kweli wanahitaji bajeti kubwa ya kushughulika na
mambo hayo?.
“Tunahitaji utashi wa kuwasadia wavuvi wetu, kwa kutoa elimu
na kufanya mazungumzo nao ya mara kwa mara, kuwatembelea maeneo yao ya kazi na kubaini matatizo yao kisha kuyafanyia kazi” Alibainisha Dk
Kamani.
Kuhusu zao la kuku, Waziri Kamani amesema sasa hivi kuna
tatizo la mayai feki na chanjo feki, alihoji ni kweli kwamba wafanyakazi wa
wizara hiyo haiwajui wahusika au kuna baadhi ya watumishi ndio miradi yao ? ambapo aliagiza
wizara kubaini wanaofanya biashara hiyo feki ambayo inaleta madhara hasa wakazi
wa mjini ambao ni watumiaji wakubwa wa bidhaa hizo.
No comments:
Post a Comment